Mabadiliko ya KRA: Kutoka Mtoza ushuru hadi Mtoaji Huduma

KRA ya kuboresha utoaji wa huduma 

Katika miaka ya hivi karibuni, Mamlaka ya Ushuru ya Kenya (KRA) imeanzisha safari ya uboreshaji katika utoaji wa huduma na kukuza mwingiliano chanya na walipa kodi. Kupitia mipango mbalimbali na maboresho, KRA imepiga hatua kubwa katika kutoa huduma kwa njia rahisi na yenye ufanisi kwa umma. Ifuatayo ni  jinsi KRA imekuwa taasisi bora kwa kuchukua hatua madhubuti za kuboresha operesheni zake na mwingiliano na raia;

Kukumbatia Teknolojia habari na Mawasiliano:

Moja ya hatua muhimu ambayo KRA imechukua ni kukumbatia teknolojia ili kusukuma mchakato na kuboresha utoaji wa huduma. Uanzishwaji wa majukwaa ya mtandaoni kama vile iTax, eTims,icms,Ibid-mnada wa forodha  na M-service (Huduma ya rununu) umefanya iwe rahisi kwa walipa kodi kuwasilisha taarifa, kufanya malipo, na kupata huduma wakati na pahali popote wakiwa  nyumbani au ofisi zao. Hatua hii ya kidijitali imeboresha ufanisi na kupunguza haja ya kutembelea ofisi za KRA, hivyo kuokoa muda na rasilimali kwa walipa kodi.

Ugatuzi wa Huduma.

Kuanzisha vituo vingi vya huduma kwa walipa kodi katika kila  jimbo (Huduma centres) kumetoa njia kwa walipa kodi kutafuta msaada na ufafanuzi juu ya masuala yanayohusiana na kodi kwa urahisi. Aidha, mamlaka ya ushuru huendesha kampeni za huduma mashinani katika maonyesho barabarani, kwa lengo la kufikia wote. Kipaumbele hiki katika huduma kwa wateja kimeisaidia kujenga imani na uaminifu kati ya walipa kodi na kuboresha mtazamo chanya kuhusu mamlaka.

Kuboresha Huduma kwa Wateja.

KRA pia imefanya maendeleo makubwa katika kuboresha huduma kwa wateja na kutoa majibu haraka kwa mahitaji ya walipa kodi. Aidha, KRA imewekeza katika mafunzo ya wafanyakazi wake, ili kutoa huduma kwa heshima na ufanisi, kuhakikisha kuwa walipa kodi wanapata msaada unaohitajika kwa wakati unaofaa. KRA inaendelea kuhamasisha washika dau kila mara kuhusu uadilifu njia za kuripoti visa vya ufisadi na utovu wa nidhamu. Aidha, Maafisa wa KRA hutakiwa kuweka wazi mgongano wa maslahi katika shughuli za utendakazi.

Kuongeza Uwazi.

Uwazi ni eneo lingine ambalo KRA imefanya maendeleo makubwa. Kwa kuchapisha taarifa kuhusu sheria za kodi, kanuni, na taratibu, KRA imeongeza uwazi kwa walipa kodi, kuwawezesha kuelewa haki na majukumu yao vizuri zaidi. Zaidi ya hayo, mipango kama vile kampeni na uhamasishaji wa umma umesaidia kufafanua mchakato wa kodi na kukuza utekelezaji kati ya raia.

Kuwezesha Utii na ulipaji kwa Hiari.

KRA imekubali umuhimu wa kuendeleza utekelezaji wa hiari miongoni mwa walipa kodi kama njia ya kufikia malengo ya mapato kwa njia endelevu. Kwa lengo hili, KRA imechukua njia ya ushirikiano na walipa kodi kupitia majadiliano, warsha, njia mbadala ya kusuluhisha migogoro na wadau ili kushughulikia wasiwasi wao na kukusanya maoni. Hili limejenga imani na uaminifu kwa walipa kodi.

Maendeleo endelevu.

 KRA imejikita katika kuimarisha uwezo wake wa taasisi ili kukidhi mahitaji ya vizazi vijavyo. Mtindo huu ni  matumizi ya rasilimali unaojali mahitaji ya sasa bila kuathiri uwezo wa vizazi vijavyo. KRA imewekeza katika mafunzo na maendeleo ya wafanyakazi wake, kuboresha miundo msingi na mifumo ya teknolojia, na kuboresha udhibiti wa ndani na miundo ya utawala.  Lengo ni kujenga shirika lenye uwezo na thabiti, hivyo basi, KRA imejiweka vizuri zaidi kutekeleza majukumu yake kwa siku sijazo.

Hitimisho

Kwa muhtasari, azma ya KRA ya kuboresha utoaji wa huduma na kukuza mwingiliano chanya na walipa kodi inaonekana katika maboresho mbalimbali na mipango iliyotekelezwa. Kupitia kidijitali, ugatuzi wa huduma, kuboresha huduma kwa wateja, uwazi, kuwezesha utii na ulipaji kwa hiari na maendeleo endelevu, KRA imepiga hatua kubwa katika kutoa huduma bora kwa njia rahisi na zenye kufikiwa kwa haraka na umma.

 

Na Nicholas Kimutai Kirui.


BLOG 04/04/2024


Did you find this content useful?

Average Rating

5
Based on 15 ratings
💬
Mabadiliko ya KRA: Kutoka Mtoza ushuru hadi Mtoaji Huduma